Miradi ndio uti wa mgongo wa taasisi zisizo za kiserikali
(NGOs), kupitia miradi taasisi huweza kujiendesha, kutimiza malengo yake ya
kimkakati (Strategic objectives) na pia kufikia uono wake (vision attainment).
Upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufadhili miradi imekuwa ni changamoto kwa taasisi nyingi na kupelekea baadhi ya
taasisi kusitisha shughuli.
Ili taasisi iweze kupata fedha kutoka kwa mfadhili kwa ajili
ya kutekeleza mradi; haina budi kuwa na ujuzi katika mbinu na matakwa yatakiwayo
na mfadhili husika. Mbinu zifuatazo endapo zitatumika ipasavyo zitaiwezesha
taasisi husika kupata fedha za mradi kutoka kwa mfadhili yeyote.
·
Kuwa na ufahamu juu ya taasisi ambazo zinatoa fedha za
miradi. Kuna taasisi za ndani kwa mfano Foundation For Civil Society, hawa
wanatoa kuanzia Shilingi milioni 20 ( kwa miradi midogo yaani Innovative
projects ya mwaka mmoja) mpaka Shilingi milioni 250 (kwa miradi mikubwa
ya miaka mitatu yaani Strategic projects),
wanafadhili miradi iliyojikita katika utawala bora (Good governance), kujengea
taasisi uwezo (CSOs capacity development) na maendeleo ya kiuchumi (Economic
development)
Kwa upande wa
taasisi za nje kuna Danish International
Development Agency (DANIDA), Agency
Francaise de Development (AFD), UK Government Department for International
Development (DFID), European Union (EU) na zingine nyingi. Baada ya kuzifahamu taasisi hizi; ni
vyema ukafahamu pia wakati gani wanaanza
kupokea maombi kwa ajili ya fedha za miradi.
·
Kuwasilisha andiko zuri la mradi (Effective project
proposal), hii ndio dira inayoonesha ni
namna gani mradi utatekelezwa na nini kinatarajiwa baada ya utekelezaji .Uwasilishaji
wa maandiko thabiti ya miradi imekuwa ni changamoto kwa taasisi nyingi hapa
nchini, maandiko mengi yanakosa uhalisia na hayapimiki (unrealistic and can’t be
measured) Kuna miundo mbalimbali katika uandaaji wa haya maandiko, na kila
mfadhili huwa na muundo anaopendekeza. Hivyo ni vyema taasisi husika ikafahamu
mfadhili anataka muundo gani katika andiko kisha kuliandaa kikamilifu na kuwasilisha.
·
Kuwa mshindani (Be competitive) upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
umejaa ushindani kwa kiasi kikubwa. Hivyo ni jukumu la taasisi husika kuibuka
mshindi katika ushindani huu ili kuweza kupata hizo fedha. Njia bora na ya uhakika
ya kuwa mshindani ni kuhakikisha unatimiza vigezo na masharti yote utakiwayo na
mfadhili; kama vile uwasilishaji wa taarifa za benki, nakala ya katiba ya
taasisi, barua ya utambulisho kutoka mamlaka za mitaa n.k, pia uwasilishaji wa
nyaraka unapaswa kufanywa mapema kabla ya muda kuisha.
·
Kuwa na ushirika madhubuti (Having an effective partnership), mashirika kama Umoja wa Ulaya (EU) mara nyingi hutoa
fedha kwa miradi ambayo inatekelezwa katika ushirika. Imekuwa ni tatizo kubwa
kwa taasisi nyingi hasa pale zinapotakiwa kuchagua taasisi-mshirika ili waweze
kupatiwa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi. Kutokana na kutojiandaa mapema
katika kutafuta mshirika sahihi, taasisi nyingi hujikuta zinashindwa kutimiza
vigezo vya kutafuta ushirika na hatimaye kukosa fedha kutoka kwa mfadhili.
·
Usimamizi madhubuti wa mradi (Effective project management),
ni bahati mbaya sana taasisi nyingi hutoa nafasi
za ajira pindi tu fedha za mradi zinapopatikana, baada ya mradi kuisha; ajira
zinafika kikomo. Hivyo taasisi kila siku hujikuta iko na watu wapya katika
kutekeleza miradi. Hali hii huifanya taasisi kutokuwa na watu wenye uelewa katika
usimamizi wa miradi inayofadhiliwa na mfadhili husika, hivyo huleta changamoto
katika ufikiaji wa matarajio ya mfadhili.
0 comments